Moshi. Jeshi la Polisi linamshikilia
dereva mmoja wa pikipiki, maarufu kama bodaboda wilayani Mwanga mkoani
Kilimanjaro baada ya mke wa askari polisi kukutwa amekufa chumbani kwa dereva
huyo.Tukio hilo ambalo limezua gumzo kubwa wilayani humo lilitokea juzi saa
12:00 jioni katika eneo la New Mwanga wilayani humo na mtuhumiwa akidaiwa
kukutwa akiwa amelewa chakari.
Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Shaibu Ndemanga
amethibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kusema uchunguzi unaendelea.“Hilo tukio
lina ukweli na bahati mbaya sana mumewe ndiyo kwanza amehamishiwa Geita na
alikuwa akaripoti halafu aje kuchukua familia yake,” alisema Ndemanga.
Mkuu huyo wa wilaya ambaye pia ni mwenyekiti
wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo, alisema hadi sasa haijafahamika
nini kilitokea na kwamba hilo ni moja kati ya mambo ambayo polisi inachunguza.“Hayo
yote kwamba ilikuwaje akawa chumbani kwa huyo kijana, nini sababu za kifo
yatajulikana kadiri upelelezi unavyoendelea,” alisema.
Imeelezwa kuwa jana ilikuwa siku ya askari
huyo kuripoti katika kituo chake kipya cha kazi.
“Mpaka sasa hivi haijajulikana nini hasa
kilitokea huko chumbani na ilikuwaje akawa chumbani kwa huyo dereva,” alisema
mmoja wa watu waliokuwapo katika eneo la tukio ambaye hata hivyo, hakutaka
kutaja jina lake na kuongeza kuwa jana saa sita mchana, mwili wa mwanamke huyo
ulichukuliwa kutoka Hospitali ya Wilaya ya Mwanga na kuhamishiwa Hospitali ya
Rufaa ya KCMC kwa uchunguzi.
Taarifa za awali zinasema kuwa mwili wa
marehemu ulikuwa na mikwaruzo shingoni hali inayotia shaka kuwa huenda
alinyongwa.
Habari nyingine zinadai kuwa siku ya tukio,
mwanamke huyo alikuwa ameaga kuwa anakwenda kanisani lakini baadaye simu yake
ilipopigwa ilikuwa ikipokewa na mwanamume.
Ilidaiwa kuwa mume wa marehemu alipojaribu
kupiga simu ya mkewe, ilikuwa ikipokelewa na mtu aliyeonekana kuwa ni mlevi wa
kupindukia hali iliyomtia wasiwasi na kuamua kuwapigia simu marafiki zake wa
karibu ili wamsaidie kumtafuta ndipo walipopata taarifa kuwa ulikuwapo uhusiano
kati ya shemeji yao na dereva huyo wa bodaboda.
Ilidaiwa kuwa marafiki hao walikwenda moja kwa
moja nyumbani kwa dereva huyo wa bodaboda ambako walimkuta akiwa amelewa na walipoingia
ndani walimkuta shemeji yao akiwa ameshafariki dunia.”
Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Robert
Boaz hakupatikana jana kuzungumzia tukio hilo kwa kuwa alikuwa kwenye ziara ya
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda huko Gonja wilayani Same.
0 Komentar untuk "KALI HII: MKE WA POLISI AFIA NYUMBANI KWA DEREVA BODABODA"